WAKAZI wa Jiji la Arusha jana asubuhi waliingiwa na hofu kutokana na milio ya mabomu ya machozi yaliyopigwa na polisi kwa lengo la kuzima maandamano ya madereva na makondakta wa daladala.
Jiji la Arusha katika siku za karibuni tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, limekuwa likikumbwa na machafuko ambayo wakati mwingine, hulazimisha polisi kutumia nguvu za ziada ikiwamo mabomu ya machozi.
Madereva na makondakta hao ambao wako katika mgomo wa kushinikiza wenzao zaidi ya 40 kuachiwa huru na kuondolewa kwa kile walichokiita sheria kandamizi za usalama barabarani, pia walisababisha shida kubwa ya usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.
Kufuatia hali kuwa tete, mnamo saa 4:00 asubuhi Jeshi la Polisi lililazimika kuzuia maandamano ya kundi la madereva wapatao 200 katika eneo la mnara wa Mwenge, baada ya kutumia mabomu ya hali iliyozua tafrani katikati ya Jiji la Arusha.
Purukushani hizo kati ya polisi na madereva hao zilitokea muda mfupi kabla maandamano hayo hayajashika kasi kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo, maandamano hayo yalizimwa baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao.Mabomu hayo ya machozi yalisababisha waandamanaji kusambaa, lakini wengi wao walielekea kwenye Barabara ya Dodoma- Arusha.
Polisi nao waliwafuata na kuzidi kuwamiminia mabomu ya machozi ya mfululizo yapatayo 15 na kuzidi kuzua tafrani kwa wakazi wa hapa, ambao wengi wao ndio walikuwa wakiingia kazini na wanafunzi kwenda shuleni.
Hali ilizidi kuwa tete jijini hapa ambako madereva hao waliamua kukusanyika katika eneo la chini ya mti na eneo la mzunguko wa Impala, ambako polisi wakiwa na magari yao walifika katika maeneo hayo na kisha kuanza kuwatangazia watanyike.
Agizo hilo la mdomo halikuwatia hofu waandamanaji hao, ambao waliendelea kujikusanya ,lakini wakati huo tayari FFU wakiwa na pikipiki na magari walikuwa wametawanyika katika maeneo mbalimbali ya viunga vya Jiji la Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alisema polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi baada ya kubaini kuwa baadhi ya watu walitaka kutumia maandamano hayo kufanya uhalifu.
Alisema polisi imewashikilia watu saba kwa uchunguzi baada ya kutokea uharibifu mkubwa wa mali madukani na kuvunjwa vioo vya magari wakati maandamano hayo.Maelfu ya wakazi wa jiji la Arusha, walionekana barabarani wakitembea kwa miguu na baadhi yao wakiwa wametoka eneo Usa River, ambalo lipo kilomita 50 nje ya Jiji.
Baadhi ya wakazi wa Arusha walisema sehemu ambayo walikuwa wakisafiri kwa Sh 2,000, walitozwa hadi Sh 8,000 kwa safari moja.