Siku moja baada ya Steven Wassira kutangaza nia ya kutetea ubunge wa Jimbo la Bunda mwakani, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya amesema anashangaa kuona mwanasiasa huyo mkongwe anaweweseka kwa kutojua ni nafasi ipi anaitaka.
Bulaya, ambaye alisema muda wa yeye kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo bado haujafika, alishangaa kuhusu hatua ya waziri huyo wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) kutangaza kugombea ubunge kuwa ni kukiuka kanuni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani Bunda juzi, Wassira (69) alitangaza nia hiyo huku akijigamba kuwa yeye ni mwarobaini wa matatizo ya wananchi wa jimbo hilo na hivyo atagombea tena ubunge mwakani.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bulaya, ambaye amekuwa akijishirikisha kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kwenye jimbo hilo ikiwa ni pamoja na kuendesha mashindano ya mpira wa miguu, alisema ingawa wazee na akina mama wa Bunda wanamwomba awanie nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu, muda wake kutangaza nia hiyo bado.
Bulaya alisema: “Mimi namshangaa Wassira kwa kutangaza kutaka ubunge wakati anatumikia adhabu aliyopewa na chama. Mimi siwezi kusema chochote sasa hivi kama nitagombea ubunge mwaka 2015 au la,” alisema Bulaya na kuongeza: “Kwa taratibu na kanuni za chama muda wa kutangaza nia bado, ndiyo maana Wassira na makada wengine walishapewa onyo walipobainika kuanza kampeni za urais,” alisema Bulaya.
Aliongeza: “Wenye haki ya kuchagua viongozi ni wananchi. Kama wananitaka wao ndiyo watanichukulia hadi fomu. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza,” alijigamba Bulaya na kufafanua kuwa upepo mzuri katika siasa ni wananchi, kama wanakuunga mkono huna haja ya kuwa na wasiwasi.”
“Mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete anataka kugombea urais, aliacha ubunge, lakini yeye mara atake urais, mara ubunge. Mtu anayejiamini hawezi kugombea nafasi mbili. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza,” alisema Bulaya.