Wezi walivamia kiwanda cha simu cha Samsung nchini Brazil usiku wa Jumatatu na kuiba mali yenye thamani ya dola milioni thelathini na sita.
Mali hiyo ilikuwa pamoja na simu za mkononi na komputa.
Genge hilo lililokuwa limejihami vikali, liliwateka wafanyakazi wanane waliokuwa wanaodnoka kazini na kuiba vitambulisho vyao ambavyo walivitumia kuweza kuingia katika kiwanda hicho mjini Sao Paulo.
Inaarifiwa wezi hao waliwazidi nguvu walinzi na kuchukua muda wa saa tatu kufanya wizi huo.
Polisi wanasema kuwa genge hilo lilikuwa na wezi, 20 ambao walifanikiwa kuiba simu 40, 000 pamoja na tarakilishi, tabiti na vifaa ningine vyenye thamani ya dola milioni 36.
Walipovamia kiwanda hicho waliamuru wafanyakazi wote kuondoa betri zao kwenye simu ili wasiweze kumpigia mtu yeyote simu.
Walifanya wizi kiwandani kwa karibu masaa matatu na walifahamu vyema ambako vifaa vyenye thanai zaidi vilikuwa vimewekwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa na kwamba kampuni hiyo haina tatizo lolote kwa sasa.
Polisi wanachunguza kanda za video kuona ikiwa wanaweza kuwatambua wezi hao.