Ni Jumatatu nyingine tunapokutana katika uwanja wetu huu murua, tukijuzana, kuelimishana na kujadiliana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Namshukuru Jalali kwa kuniwezesha kuiona tena siku hii, naamini na wewe msomaji wangu uko poa kabisa.
Mfumo wa maisha ya familia nyingi siku hizi unawalazimu wahusika kutafuta wafanyakazi wa ndani (mahausigeli) kwa ajili ya kuwasaidia kazi. Ni uamuzi mzuri kwa sababu hurahisisha kazi ya kutunza familia na wengi huwa msaada mkubwa, achilia mbali wale wachache wenye tabia zisizofaa.
Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, vilio vya wanawake waliopo kwenye ndoa kulalamika kuibiwa waume zao na wasichana wa kazi vinazidi kuongezeka. Katika kila wanawake kumi wanaoishi na wasichana wa kazi, saba waliwahi kutendwa kwa waume zao kusaliti ndoa na mahausigeli au kujaribu kuwashawishi wavunje nao amri ya sita. Wanawake wengi ambao wapo katika uhusiano rasmi watakuwa mashahidi wa hili.
Yaani unaenda kumchukua dada wa kukusaidia kazi za nyumbani kijijini, unamleta mjini, unamhudumia kwa kila kitu, anaanza kuoga na kupendeza na mwisho unajikuta ukisaidiwa hata yale ambayo hukuomba kusaidiwa au ambayo hayastahili kuwa na msaidizi.
Wanawake wengine wanajeruhiwa zaidi baada ya waume zao kuishia kuwapa mahausigeli ujauzito au kuzaa nao! Dada wa kazi anageuka na kuwa mke mwenzio. Zipo sababu nyingi zinazosababisha tatizo hili na ningependa tuzijadili kwa pamoja.
1. KUJISAHAU
Wanawake wengi wana kawaida ya kujisahau wanapopata wasichana wa kuwasaidia kazi. Kama kipindi cha nyuma kabla hajapata hausigeli mwanamke alikuwa akimfulia mumewe, kumuandalia chakula kizuri na kutunza vizuri familia, akishapata dada wa kazi, hujisahau na kuacha kutimiza wajibu wake kama mke.
Wanawake wengi wana kawaida ya kujisahau wanapopata wasichana wa kuwasaidia kazi. Kama kipindi cha nyuma kabla hajapata hausigeli mwanamke alikuwa akimfulia mumewe, kumuandalia chakula kizuri na kutunza vizuri familia, akishapata dada wa kazi, hujisahau na kuacha kutimiza wajibu wake kama mke.
Matokeo yake, unakuta dada wa kazi ndiyo anashughulikia mambo yote muhimu yanayomhusu mume kuanzia anapoamka asubuhi mpaka usiku. Ndiyo! Mumeo akiamka asubuhi, dada wa kazi ndiyo anaenda kutandika kitanda, anamuandalia maji ya kuoga, anamuandalia kifungua kinywa na kumnyooshea nguo za kuvaa siku hiyo.
Mchana au jioni akirudi, yeye ndiyo anampokea, anamuandalia maji ya kuoga kisha anamuandalia chakula cha usiku. Yeye ndiye anayefua nguo zote za mumeo, hata zile ambazo hastahili kuzifua. Unategemea katika mazingira kama haya nini kitatokea kama siyo mumeo kuanza kumpenda hausigeli?
2. UKARIBU ULIOPITILIZA
Suala lingine ambalo linawaponza wanawake wengi waliopo kwenye ndoa, ni kuruhusu waume zao wawe na ukaribu wa kupitiliza na mahausigeli. Kutokana na ubize wa kazi au mtindo wa maisha, unakuta mwanamke anakuwa bize na mambo yake mengine na kusahau wajibu wake wa msingi wa kuwa karibu na mumewe.
Suala lingine ambalo linawaponza wanawake wengi waliopo kwenye ndoa, ni kuruhusu waume zao wawe na ukaribu wa kupitiliza na mahausigeli. Kutokana na ubize wa kazi au mtindo wa maisha, unakuta mwanamke anakuwa bize na mambo yake mengine na kusahau wajibu wake wa msingi wa kuwa karibu na mumewe.
Kwa mfano, usiku mama anawahi kwenda kulala kwa kisingizio cha uchovu na kumuacha mumewe na hausigeli wanatazama runinga pamoja sebuleni. Au unakuta asubuhi, mama wa familia anawahi kuondoka kabla ya mumewe na kuacha mwanya wa wawili hawa kuwa karibu na kuzoeana.
Jioni pia, baba anawahi kurudi nyumbani lakini akifika, mkewe anakuwa bado hajarudi au hata kama amerudi, yuko bize na mambo mengine kabisa. Hakuna mtu anayependa kukaa na upweke kwa hiyo kwa sababu umeshindwa kutimiza majukumu yako, taratibu atahamishia ukaribu kwa dada wa kazi, watazoeana na kuanza kuvukiana mipaka.
Unategemea mwisho utakuwa ni nini?Tukutane wiki ijayo kuangalia ni mambo gani unayopaswa kuyafanya ili kuondoa kabisa mianya ya kuibiwa mumeo na hausigeli wako. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.