Zanzibar, Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Muhamed Khatib
Mkombalaguha amefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa vibaya baada ya
kurushiwa bomu na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limetokea katika eneo la Darajani muda
mfupi baada ya maelfu ya wakazi wa zanzibar kuhudhuria mawaidha
yaliyokuwa yakitolewa na Sheikh Kassim Mafuta Kassim mkazi wa Pongwe Mkoani Tanga.
Taarifa rasmi kutoka kwa Naibu Mkurugenzi wa
Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI) Yusuph Ilembo zimefafanua
kuwa Tukio hilo limetokea majira ya saa mbili na nusu usiku wa kuamkia
leo na bomu hilo lilirushwa kwa mkono na watu wasiojulikana wakati
waumini wakiagana na mtoa mawaidha Sheikh Kassim katika eneo la kuegesha
magari Darajani visiwani Zanzibar.
DDCI Ilembo pamoja na kuthibitisha kutokea kwa
tukio hilo amesema jeshi la polisi tayari limeanzisha operesheni maalum
ya kuwasaka watu waliohusika na shambulio hilo kwa kushirikiana na
vikosi vingine vya ulinzi na usalama visiwani hapa.
“Mlipuko huu pia umesababisha gari
mbili zilizokuwepo katika eneo la tukio kuathirika, tumeanza kufanya
uchunguzi ingawa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa hadi hivi sasa “ alisema
DDCI Ilembo.