KIPA wa zamani wa mabingwa wa England, Chelsea FC, Vincent Atchouailou de Paul Angban anatarajiwa kuwasili wiki ijayo kwa ajili ya kusaini Mkataba wa kujiunga na Azam FC.
Mlinda mlango huyo aliyezaliwa Februari 2, mwaka 1985 mjini Anyama, kwa sasa anadakia klabu ya Ligi Kuu ya kwao, Ivory Coast, Jeunesse.
Habari kutoka ndani ya Azam FC, zinasema kwamba mazungumzo ya awali yamekwishafanyika baina ya klabu na kipa huyo na amekubali kuja kufanya kazi Chamazi.
Vincent Angban aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Chelsea chini ya umri wa mika 21 ingawa alikuwa amevuka umri huo katika harakati za kutafuta kusajiliwa The Blues, lakini pamoja na kuonyesha uwezo Stamford Bridge, haikuwa bahati yake jezi ya bluu.
Angban akiwa na Fernando Torres wakati walipokuwa Chelsea, sasa anakuja kufanya kazi Chamaz
Kipa huyo aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.
Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah.
Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.
Baada ya kumaliza Mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U21 ya Chelsea.
Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwemo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi na Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.
Azam FC inamchukua kipa huyo kwa lengo la kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Afrika- na kama inavyojulikana timu hiyo ya bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake mwakani itacheza Kombe la Shirikisho.
Mzuia michomo hatari, Angban anahamishia makali yake Chamazi
Akisani Azam FC, kipa huyo atakwenda kugombea namba na makipa wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ali.
Kabla ya kuanza kwa ligi ya Bara hapo Agosti 22 mwaka huu, Azam pia imeshaanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambayo yatafanyika nchini mwezi ujao.
Usajili wa kipa huyo ukikamilika, Azam itakuwa na wachezaji wanne kutoka Ivory Coast, wengine ni Serge Wawa Pascal na pacha, Kipre Herman Tcheche na Kipre Michael Balo