Tanga\Dodoma. Harakati za makada wa CCM wanaowania urais kusaka wadhamini mkoani zinaendelea kukumbwa na vituko baada ya wanamgambo wa chama hicho, maarufu kama Green Guards, kumshushia mkong’oto Dk Mussa Muzamill Kalokola aliyeingilia mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya mgombea mwingine.
Tukio hilo lililotokea juzi, ni mwendelezo wa matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mchakato huo, yakiwamo ya wanachama kutaka kuchana fomu za mgombea baada ya kunyimwa ‘posho’ na kada mwingine kukosa wadhamini na kulazimika kuomba chakula cha mchana kutoka kwa mkuu wa wilaya.
Katika tukio la Tanga, Dk Kalokola, ambaye pia anadaiwa kushawishi wanachama wasimdhamini mgombea mwingine wa urais, Bernard Membe, alidaiwa kuvamia mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kutaka kulazimisha apewe kipaza sauti kwa ajili ya kuomba wanachama wamdhamini, kitu ambacho viongozi wa CCM wa wilaya hawakukubaliana nacho na alipoendelea kung’ang’ania ndipo Green Guards walipoamriwa wamuondoe eneo hilo.
Picha za video za tukio hilo ambazo zimesambazwa mitandaoni zinawaonyesha vijana hao wa Green Guards wakimsomba mzobemzobe mgombea huyo, kumuangusha kwa kumpiga ngwala na mkoba wake wenye stika ya fomu za mgombea urais, ukionekana kuzagaa chini.
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mkasa huo, Dk Kalokola alikiri kupigwa katika tukio hilo lilitokea mchana Jumatano ya Juni 17, 2015 alipofika kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Tanga Mjini, siku ambayo mgombea huyo anadai alipangiwa na katibu wa wilaya.
Dk Kalokola alisema baada ya kukabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa na CCM Julai 15 mwaka huu mkoni Dodoma, alikwenda mkoani Tanga ili kupata wadhamini.
“Tulielekezwa kuwa makatibu wa CCM wa mikoa ndiyo watakaotutafutia wadhamini siyo sisi tutafute hivyo mimi tarehe 16 nilikwenda ofisi za CCM kuripoti kwa katibu wa Mkoa,” alisema.
Hata hivyo, alisema hakuweza kuonana na Katibu huyo baada ya kuambiwa kuwa hayupo na amemwachia majukumu hayo katibu wa CCM wa Wilaya ya Tanga Mjini.
Alisema siku hiyo alikuta wagombea wawili waliofika ofisi hizo wakitaka kupewa wadhamini ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Balozi Amina Salum Ali.
“Hawakutaka hata kunisikiliza shida yangu. Mimi nikaamua kutoa taarifa makao makuu ya CCM,” alisema.
Hata hivyo, baadaye saa 12:00 jioni alipigiwa simu na katibu wa CCM wilaya hiyo ya Tanga, akielezwa kuwa aende siku inayofuata asubuhi yaani Alhamisi.
“Nilienda pale nikasaini kitabu nikawaeleza kuwa mimi jana (juzi) nilikuwa na kesi ya kupinga Katiba jijini Dar es Salaam kwa hiyo ningeomba nipate wadhamini siku hiyo hiyo ili nisafiri,”alisema Dk Kalokola ambaye amefungua kesi akitaka Mahakama Kuu itangaze kuufuta mchakato wa kupata Katiba mpya kinyume cha utashi wa chama hicho tawala ambacho kinajisifu kwa kufanikisha mchakato huo.
SOURCE: MWANANCHI