Dodoma. Moto wa uchaguzi mkuu umezidi kupamba baada ya mtandao wa walimu vijana nchini kujitokeza hadharani na kuahidi kumpigia kampeni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba katika safari yake ya kuwania urais.
Pia, mtandao huo uliahidi kuwafanyia kampeni Makamba na vijana wenzake wote watakaojitokeza kuwania ngazi mbalimbali za uongozi bila kujali itikadi za vyama vyao iwe CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi au chama kingine chochote hadi ndoto yao ya vijana kujiongoza na kujitawala itakapotimia.
Walimu hao walikusanyika jana katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Umonga mjini Dodoma pamoja na kuzindua uanzishwaji wa mtandao huo, walitangaza kumuunga mkono Makamba.
Akisoma tamko la mtandao huo, Mwenyekiti wake, tawi la Dodoma, Fredrick Mwakisambwe, alisema mtandao huo, unamuunga mkono Makamba kwa sababu ni mzalendo, mwadilifu na ana uwezo kuongoza.
“Na tunawahimiza na kuwahamasisha vijana wengine wengi zaidi wajitokeze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo uenyekiti wa Serikali za Mitaa, vijiji, udiwani na ubunge.”
Alisema ni wajibu wao kuwakumbusha Watanzania kwamba Taifa hili lilikombolewa na ndio maana kiongozi wa kwanza wa Taifa hili alikuwa mwalimu tena kijana akiwa na umri wa miaka 39 tu.
Sisi walimu vijana kupitia huu mtandao wetu bila kuuma maneno tunasema tunataka Taifa letu liongozwe sasa na kiongozi mwenye kuendana na changamoto za kizazi hiki, mwenye fikra za hiki kizazi,” alisema