Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Mike Okoth amesema hatamzuia mwanawe Divorc Origi kujiunga na Liverpool kwa kitita cha pauni milioni kumi.
Lakini Okoth amesema watajadialiana mambo kadhaa pamoja na timu zingine ambazo zinataka kumsajili Origi ambaye aliiwakilisha Ubelgiji kwenye mashindano ya kombe la dunia nchini Brazil.
Mbali na Liverpool timu zingine za ligi kuu ya England ambazo zimeonyesha nia ya kumsajili Origi ni Tottenham Hotspur na Arsenal lakini hawajataja kiasi cha fedha mbazo wako tayari kutoa.
Akizungumza na BBC Jumatatu wiki hii kwa njia ya simu akiwa Ubelgiji, Okoth, ambaye alihudhuria mashindano ya kombe la dunia anasema:”
Okoth amesema kuwa bado anamsubiri kijana arudi kutoka Ubelgiji kisha azungumze naye.
''Yeye ni mtu mzima mwenye uwezo wa kujiamulia mengine. Kuna timu kutoka Ujerumani, Italia na Hispania ambazo zimewasiliana nasi kupitia wakala wao.Itabidi tuchunguze uzito wa timu hizo na makocha wanaozifunza,’’ alisema babake Origi.
Babake Origi, Mike Okoth
'Klabu ya kumkuza Origi'
Katika mashindano hayo yanayomalizika Jumapili hii, Origi aliiwezesha Ubelgiji kufuzu kwa raundi ya pili alipofunga bao na kuilaza Urusi 1- 0. Aliingia katika kipindi cha pili na kuchukua nafasi yake Romelu Lukaku.
''La mhimu ninalotaka ni ajiunge na klabu itakayomkuza na apate fursa nzuri ya kujiendeleza. Sitafurahia ajiunge na klabu ambayo hatapata muda wa kutosha wa kucheza hata kama pesa ni nyingi. Siangalii tu pesa lakini nalenga mbele kimchezo.Anaweza kujiunga na klabu inayotoa pesa nzuri za kuhama lakini singetaka mara tu akivuka aanze kujuta kama hachezi mara kwa mara.’’
Kwa sasa Origi anaichezea Lille ya Ufaransa lakini anasema lengo lake kubwa ni kushiriki ligi kuu ya England.
Okoth anasema licha ya kwamba yeye ni shabiki wa Liverpool watazungumzia zaidi mambo mengine na Origi akirudi Ubelgiji kutoka Brazil ambako aliiwakilisha taifa lake alikozaliwa na kufurahisha wengi wakiwemo mashabiki wa Kenya ambao baadhi yao walibubujikwa na machozi Ubelgiji ilipong’olewa na Argentina kwenye mechi ya robo-fainali ambayo walipoteza kwa bao 1-0.