Klabu ya Ligi Kuu ya soka ya England – Premier League Liverpool, imemsaini kiungo chipukizi wa Bayer Leverkusen Mjerumani Emre Can mwenye umri wa miaka 20. Uhamisho huo umethibishwa na vilabu viwili
Can ameichezea Leverkusen mechi 39 katika vinyang'anyiro vyote tangu alipojiunga nao msimu uliopita. Can mzaliwa wa Frankfurt, mwenye asili ya kituruki, na anayeweza pia kucheza kama beki, alijiunga na Leverkusen kutokea Bayern Munich msimu uliopita, na kuwasaidia kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Bundesliga na kufuzu pia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwingineko, mshambuliaji wa Japan Yuya Osako amejiunga na klabu ya FC Cologne iliyopandishwa daraja katika Bundesliga msimu ujao. Osako mwenye umri wa miaka 24, ametokea klabu ya 1860 Munich. Mshambuliaji huyo, ambaye yuko katika kikosi cha Japan kinachojiandaa kwa dimba laKombe la Dunia, atasaini mkataba utakaomfikisha Juni mwaka wa 2017.
Mkataba huo umefanyika baada ya nahodha wa Japan Makoto Hasebe kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu nyingine ya Bundesliga Eintracht Frankfurt kutoka Nuremberg iliyoshushwa daraja. Klabu nyingine ya Bundesliga iliyofanya biashara ni Hertha Berlin iliyomsajili Mjapan Genki Haraguchi. Haraguchi mwenye umri wa miaka 23, anajiunga na Mjapan mwenzake katika klabu hiyo ya Berlin iliyomaliza katika nafasi ya 11 msimu uliopita.